Pages

Friday, May 4, 2018

JIFUNZE JINSI YA KUANDIKA CV IKIWA HAUNA UZOEFU WA KAZI

Posted by   on


JIFUNZE JINSI YA KUANDIKA CV IKIWA HAUNA UZOEFU WA KAZI
Umemaliza masomo, sasa ni wakati wako wa kurudi ´uraiani´ na kutafuta kazi. Kufanikisha hili, unahitaji uwe na CV itakayo kuuza kwa waajiri, itakayoonyesha elimu, ujuzi, maadili ya kazi na jinsi gani utakuwa mfanyakazi unayejituma.
Lakini sasa, unaposoma matangazo mengi ya kazi katika tasnia yako unajikuta unakidhi vigezo vingi vilivyowekwa isipokuwa kile cha ‘uwe na uzoefu wa kazi usiopungua muda flani’, na kujikuta njia panda kutokana na ukweli kwamba;
¨Unahitaji kazi ili kupata uzoefu, lakini ukihitajika uwe na uzoefu ili kupewa kazi.¨
Kwa bahati nzuri, uzoefu ambao waajiri wengi wanauhitaji haupatikani tu kupitia ulimwengu wa ajira rasmi.
Siri kubwa ya uandishi wa CV pasipo kuwa na uzoefu wa ajira rasmi upo katika kuonyesha kuwa una ujuzi unaoweza kuhamishika kwaajili ya kazi unayoiomba na uwezo wa kumshawishi mwajiri kutazama zaidi kile unachoweza kufanya kuliko kile ambacho umeshawahi kufanya.
Hivyo basi, unaweza vipi kuwasilisha CV yako bila ya uzoefu wa kazi? Fanya yafuatayo;
1. ONYESHA UWEZO WAKO
Kama nilivyotangulia kusema, waajiri hawaangalii tu kile ulichokifanya lakini pia unachoweza kufanya. Hivyo ni lazima uwashawishi kuwa una uwezo wa kumudu kazi unayoiomba.
Ikiwa wewe ni mhitimu jiulize, je ulifanya mafunzo kwa vitendo (field/practical training/internship) wakati wa masomo yako? Je, umeshawahi kufanya kazi katika kampuni au biashara ya rafiki, ndugu au jamaa hata kwa muda mfupi au kwa kujitolea?
Unaweza kabisa kutumia vitu hivyo kuonyesha una uzoefu flani wa kazi.
2. ANZA CV YAKO KWA TAARIFA BINAFSI
Hii itakuwa sehemu ya kwanza kabisa mwajiri yoyote kuisoma, hivyo hakikisha haina makosa, fupi na rahisi iwezekanavyo.
Sehemu hii ni mahsusi kwaajili ya kutoa sifa ulizonazo kwa kazi unayoiomba. Hakikisha unajikita zaidi kwenye kuonyesha sifa (competencies/qualifications) zako zinazoendana na ambazo mwajiri anazihitaji kwa mtu wa kushika nafasi husika.
Unaweza pia kuongeza shahada au masomo uliyoyasoma ukiwa chuo endapo yanaendana na kazi au yataongeza mvuto kulingana na aina ya majukumu katika kazi unayoomba.

3. ORODHESHA UJUZI BADALA YA MAJUKUMU
Tengeneza orodha ya ujuzi wako, na uonyeshe kwa mifano. Ikiwa unataka kusema una ujuzi wa uongozi, basi unaweza kuzungumza kuhusu tukio uliloliandaa au kulisimamia wakati ukiwa masomoni au kwenye field.
Lakini pengine wewe ni mzuri katika mawasiliano, basi toa mfano wa jinsi gani hili lilikusaidia katika masomo yako na jinsi gani unadhani litakusaidia katika kazi.

4. ELEZA MAFANIKIO YAKO
Ongea kuhusu mafanikio yako katika mazingira tofauti kama vile utafiti, masomo au kazi za kujitolea yanayoendana na sifa za kazi unayoomba. Kwa kuzungumza juu ya mafanikio yako unathibitisha kiwango cha ujuzi na uwezo wako.
Pia, onyesha ufahamu na uelewa wako kuhusu maswala yanayotokea katika sekta ya kazi unayoomba na orodhesha majarida uliyowahi kusoma, midahalo au majadiliano ya ana kwa ana au kwa mtandao uliyowahi kushiriki.

5. ZIFANYE SHUGHULI ZAKO ZA ZIADA KAMA KAZI.
Kwa sababu tu ulifanya shughuli yoyote bila kulipwa haimaanishi kuwa haukupata ujuzi wowote ule muhimu. Yaweke majukumu yako ya kazi za kujitolea sawa na majukumu ya ajira – onyesha muda ulioutumia, majukumu uliyofanya na ujuzi ulioupata.
Panga majukumu uliyoyafanya kutokana na vipaombele vya mwajiri, mfano, kama unaomba kazi ya uandishi katika gazeti, mwajiri atahitaji kufahamu zaidi kuhusu makala ulizowahi kuandika kwenye majarida/magazeti kuliko uhodari wako katika michezo.
Hivyo, kuwa mwangalifu juu ya shughuli gani unaziweka kwenye CV yako, ni vizuri iendane na kazi unayoiomba.

6. CHEZA VEMA NA ELIMU YAKO.
Ikiwa uliandika utafiti (research) kama sehemu ya masomo yako, basi unaweza kuzungumza juu ya uwezo wako wa kufanya utafiti. Ikiwa ulifanya mawasilisho (presentation), pia unaweza kudai kuwa na uzoefu wa kuzungumza mbele za watu.
Jumuisha pia, uzoefu ulioupata katika mradi wa kikundi au timu (group/team project), kama vile uwezo wa kupanga, au ujuzi wowote unaohusiana na jukumu lako katika mradi.
Mwisho kabisa, wahitimu wengi hushindwa kuelezea sifa na ujuzi wao kwa namna ambayo ina ushawishi kwa waajiri kwa kushindwa kueleza vema jinsi ambavyo ujuzi walionao unaweza kuisaidia kampuni au taasisi husika.
Unakuta mhitimu anaandika kuhusu utafiti aliofanya masomoni ambao maudhui yake pengine hayaendani na majukumu atakayopewa, badala ya kuonyesha jinsi ujuzi wa kufanya utafiti utakavyo muwezesha kuandika nyaraka au ripoti zitakazo ongeza ufanisi kwenye idara mbalimbali za kampuni/taasisi.
Msingi wa CV bora kwa mtu asiye na uzoefu wa kutosha (na hata kwa wenye uzoefu) ni kuzingatia kuhusianisha kile anacho kifahamu au kuwa na ujuzi nacho, na sifa anazozihitaji mwajiri kwaajili ya kazi anayoiomba.
Hivyo, vaa viatu vya mwajiri wakati unaandaa CV yako na ujikite kwenye kuonyesha una sifa au ujuzi wa mtu ambaye mwajiri angependa kumuajiri kwa kazi husika.
        ===========================================
Kwa maelezo zaidi na mahitaji ya kutengezewa cv
Call/SMS/WhatApp “ +255764228384 …..Call/SMS +26265900071

No comments:
Write comments

Habari,zote'Mpya,Tembelea Blog yako kongwe ya NIJUZE NEWS. AU'BOFYA- https://nijuzenews.blogspot.com
Taarifa za Ajira E-mail yako